- July 5, 2026
Mhe. Balozi Henry Wambuma Ashiriki Ufunguzi wa Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Lugha ya Kiswahili Jijini Bujumbura
Mhe. Balozi Henry Wambuma, Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Burundi, tarehe 5 Julai 2026 alishiriki katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 3 wa Kimataifa wa Lugha ya Kiswahili, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Donatus, jijini Bujumbura.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Burundi. Hafla ya ufunguzi iliongozwa rasmi na Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Mhe. Bi. Lydia Nsekera, ambaye aliwakaribisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Balozi Wambuma aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Burundi kwa maandalizi mazuri na kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu. Alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya Burundi katika kukuza lugha ya Kiswahili na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia lugha hiyo.
Balozi Wambuma alisisitiza umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya mshikamano, mawasiliano na utambulisho wa wananchi wa Afrika Mashariki. Alieleza matarajio yake ya kuona Kiswahili kikitumiwa kikamilifu na kuunganishwa katika mifumo ya elimu, utawala, biashara na shughuli nyingine za kijamii katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alibainisha kuwa matumizi mapana ya Kiswahili yataendelea kuimarisha ujumuishaji wa kikanda, kurahisisha mawasiliano na kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa ukanda huu.
Aidha, aliwatakia washiriki wa mkutano majadiliano yenye tija na mafanikio, akieleza matumaini yake kuwa mapendekezo yatakayojadiliwa yatachangia maendeleo ya lugha ya Kiswahili na kuongeza nafasi yake katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Mkutano huo umewaleta pamoja mawaziri, maafisa wakuu wa serikali, wasomi, watafiti, wataalamu wa teknolojia, walimu wa Kiswahili, pamoja na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Washiriki wanajadili mikakati ya kuendeleza, kukuza na kutumia Kiswahili katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, biashara, teknolojia, utamaduni na diplomasia.
Mkutano wa Kimataifa wa Lugha ya Kiswahili unaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha hadhi ya Kiswahili kama lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mojawapo ya lugha zenye mchango mkubwa katika kuendeleza mshikamano, utamaduni na maendeleo endelevu katika bara la Afrika.



